Jumanne 3 Novemba 2026 - 08:08
Enzi ya watawala wa kusini mwa Ghuba ya Uajemi kuendelea kuziamini Marekani na Ulaya imekwisha

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi (Majlis-e Khobregan-e Rahbari), akisisitiza kwamba; Mwenyezi Mungu hutekeleza kanuni mbili mbele ya watawala madhalimu, ambazo ni kuwapa muhula na kuwakamata kwa ajili ya kuwahukumu, amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuzingatia vigezo vya kidini, kwa miaka mingi imekuwa ikiwakumbusha watawala wa eneo hili waache kuwadhulumu, kuwafedhehesha na kuwakandamiza wananchi wao, kwa sababu enzi ya kutegemea nguvu za Marekani na Ulaya imekwisha.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Mohsen Araki, Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi, katika hafla ya kumuenzi Hujjatul-Islam wal-Muslimin Haj Sheikh Hussein al-Matouq, iliyofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa Idara Kuu ya Uenezi wa Kiislamu ya Mkoa wa Qum Iran, akizungumzia kanuni za Mwenyezi Mungu katika kukabiliana na watawala madhalimu na hatima ya tawala dhalimu, alisema: Mwenyezi Mungu Mtukufu hutekeleza kanuni mbili za msingi kuhusiana na watawala madhalimu, nazo ni kanuni ya «Imhal» (kuwapa muhula) na kanuni ya «Akhidh» (kuwakamata, kuwachukulia hatua na kuwahukumu).

Kanuni ya kuwapa muhula; fursa ya Mwenyezi Mungu kwa watawala kurejea kutoka katika njia ya dhuluma

Alieleza kwamba kanuni ya kuwapa muhula ni miongoni mwa madhihirisho ya rehema ya Mwenyezi Mungu, na kuongeza: Katika kisa cha Nabii Musa na Harun (as), Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwaamuru Mitume hao wawili wazungumze na Firauni kwa upole na unyenyekevu, huenda akapata mawaidha na kurejea kutoka katika njia ya uasi na ukaidi.

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza za Kielimu, akirejelea aya tukufu isemayo:

«اذْهَبا إِلَیٰ فِرْعَوْنَ إِنَّهُ طَغَیٰ فَقُولَا لَهُ قَوْلًا لَیِّنًا»

“Enyi wawili, nendeni kwa Firauni; hakika yeye amepichuka mipaka, basi semeni naye maneno ya upole.”

Alibainisha: Aya hii inaonesha kwamba hata katika kukabiliana na mtawala kama Firauni, ambaye alikuwa amefikia kiwango cha juu kabisa cha uasi na dhuluma, Mwenyezi Mungu kwanza humfungulia fursa ya kupewa mawaidha na kurejea katika njia iliyonyooka.

Ayatullah Araki alisisitiza: Kanuni ya kuwapa muhula haiwahusu watawala madhalimu pekee, bali inawahusisha pia wafuasi na washirika wao. Hii ni kwa sababu wale wanaonyamaza mbele ya dhuluma za watawala na kwa kushirikiana nao wanachangia kuendeleza dhuluma hizo, wanakuwa washirika wao katika uhalifu na dhambi.

Wafuasi wa watawala madhalimu wanashirikiana nao katika hatima yao

Mjumbe wa Baraza la Kutambua Maslahi ya Mfumo, akirejelea aya za Qur'ani Tukufu zinazozungumzia mazungumzo baina ya viongozi dhalimu na wafuasi wao Siku ya Kiyama, alisema: Qur'ani Tukufu inasisitiza kwamba Siku ya Kiyama, watawala madhalimu na wafuasi wao watakuwa pamoja ndani ya Moto wa Jahannamu, na wafuasi hao watawapinga viongozi wao kwa kusema kwamba nyinyi ndio mliotupoteza na kutufikisha katika hatima hii.

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi, akisoma aya tukufu isemayo:

«قَالَتْ أُخْرَاهُمْ لِأُولَاهُمْ رَبَّنَا هَٰؤُلَاءِ أَضَلُّونَا فَآتِهِمْ عَذَابًا ضِعْفًا مِنَ النَّارِ قَالَ لِکُلٍّ ضِعْفٌ وَلَٰکِنْ لَا تَعْلَمُونَ»

“Na kundi lao la mwisho litawaambia kundi lao la kwanza: Mola wetu! Hawa ndio waliotupoteza, basi wape adhabu maradufu ya Moto. Atasema: Kila mmoja wenu atapata adhabu maradufu, lakini nyinyi hamjui.”

Alisema: Mwenyezi Mungu anajibu ombi hilo kwa kusema kwamba adhabu ya makundi yote mawili itakuwa maradufu; kwa sababu watawala walikuwa na mchango katika kutenda dhuluma na kuwapoteza wananchi, na vilevile wafuasi wao, kupitia ukimya, ushirikiano na uungaji mkono wao, walichangia kuendeleza dhuluma hiyo.

Kwa hiyo, wajibu wa kijamii wa watu mbele ya dhuluma na watawala dhalimu ni wajibu mkubwa, na hakuna mtu anayeweza kujiondoa katika matokeo ya kushirikiana na madhalimu kwa kujificha nyuma ya ukimya na kutokuwa na msimamo.

Muhula wa Mwenyezi Mungu si wa kudumu; shinikizo na faraja vinaweza kuwa sababu za kuamka au kuzama zaidi katika ghafla

Ayatullah Araki, akifafanua vipengele mbalimbali vya kanuni ya kuwapa muhula, alisema: Kuwapa muhula Mwenyezi Mungu Mtukufu watawala na jamii hufanyika kwa mujibu wa sheria na utaratibu maalumu, na hakumaanishi kuwa amewaacha bila kuwajibika au ameidhinisha mwenendo wao. Wakati mwingine, ndani ya mfumo wa kanuni hii, mataifa hukumbwa na shinikizo na matatizo ili yaamke kutoka katika usingizi wa ghafla na kurejea katika kutekeleza wajibu wao. Hata hivyo, wakati mwingine hali huenda kwa namna tofauti, na pale mataifa yanapokataa kujisalimisha kwenye hukumu za Mwenyezi Mungu mbele ya shinikizo hizo na kutotekeleza wajibu wao, hali na mazingira ya maisha yao huboreka ili wazame zaidi kwenye kughafilika.

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi, akisisitiza kwamba; hali zote mbili zinaweza kuwa ndani ya mfumo wa kanuni za Mwenyezi Mungu, alibainisha: Kanuni ya kuwapa muhula daima huambatana na mawaidha na maonyo kutoka kwa wanazuoni, Mitume na watu wanaojali maslahi ya jamii. Wanazuoni wa dini katika kipindi chote cha historia wamekuwa na wajibu wa kuwakumbusha watawala kuhusu tabia na utendaji wao, na kuwazuia kuendelea na njia ya dhuluma.

Akizungumzia wajibu wa wanazuoni mbele ya watawala, aliongeza: Kama ambavyo katika zama zilizopita wanazuoni wa dini walikuwa wakichukua msimamo mbele ya watawala madhalimu na kuwaonya, vivyo hivyo, leo wajibu huu bado uko juu ya mabega ya wanazuoni na shakhsia za kidini na kijamii. Inapaswa kufahamika kwamba muhula wa Mwenyezi Mungu si wa kudumu, na fursa hii itakapomalizika, itatekelezwa kanuni nyingine ya Mwenyezi Mungu ambayo ni kanuni ya kuwakamata na kuwachukulia hatua.

Maonyo ya Jamhuri ya Kiislamu kwa watawala wa eneo hili yanatokana na vigezo vya kidini

Akizungumzia sera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na watawala wa eneo hili, alisema: Kwa zaidi ya miaka arobaini, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kutegemea kanuni hii ya Mwenyezi Mungu, imekuwa ikiwatahadharisha watawala wa baadhi ya nchi za eneo hili na kuwalingania warejee kutoka katika njia ya dhuluma na wazingatie haki za wananchi wao.

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi, akirejelea aya tukufu zisemazo:

«فَذَکِّرْ إِنْ نَفَعَتِ الذِّکْرَیٰ»

“Basi toa mawaidha ikiwa mawaidha yatafaa.”

Na:

«سَیَذَّکَّرُ مَنْ یَخْشَیٰ»

“Atapata mawaidha yule anayemcha Mwenyezi Mungu.”

Alisisitiza: Sera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika suala hili imejengwa juu ya vigezo na misingi ya kidini, na lengo lake ni kuwapa mawaidha watawala na kuweka mazingira ya wao kurejea katika njia ya uadilifu na kuheshimu haki za wananchi.

Akizungumza na watawala wa nchi za eneo hili, alisema: Nchi hizi katika historia yake zimekuwa na wanazuoni na wanafikra wakubwa, na hata leo wananchi wake wana uwezo mkubwa wa kielimu, kiutamaduni na kiakili wenye thamani kubwa. Watawala wanapaswa kufahamu kwamba wananchi wao ni watu walioamka, wenye uelewa na fikra, na hawapaswi kuwanyima haki zao za kimaumbile na kijamii kwa njia ya dhuluma, udhalilishaji na ukandamizaji.

Kufungwa kwa wanazuoni, wanafikra na watu wenye vipaji kwa kosa la kutoa maonyo kwa serikali

Ayatullah Araki, akikosoa hali ya uhuru wa kijamii na namna shakhsia za kielimu na kiutamaduni wanavyotendewa katika baadhi ya nchi za eneo hili, alisema: Leo, watu wengi mashuhuri wa mataifa haya, kuanzia wanazuoni wa dini na wasomi wa vyuo vikuu hadi wahutubiaji, washairi na waandishi mahiri, wako gerezani. Katika nchi kama Kuwait, Bahrain, Saudi Arabia na Imarati, watu wamekabiliwa na vikwazo na kufungwa jela kwa sababu moja maalumu, nayo ni kuionya serikali na kueleza madai na kuwakosoa watawala.

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi, akizungumzia historia ya mapambano ya wanazuoni wa dini katika nchi za eneo hili, alibainisha: Katika kipindi chote cha historia, wanazuoni wamekuwa wakivumilia kifungo na matatizo yanayotokana na kusimama kidete dhidi ya dhuluma. Wanazuoni wa Bahrain na shakhsia kubwa za kidini nchini Saudi Arabia na Kuwait pia ni miongoni mwa watu waliokabiliwa na shinikizo na vikwazo vingi katika njia hii. Kuwakabili wanazuoni na wanafikra kwa sababu ya kueleza ukweli na kuwaonya watawala hakutatui tatizo lolote, bali kutazidisha pengo kati ya serikali na wananchi.

Kumalizika enzi ya watawala wa kusini mwa Ghuba ya Uajemi kuendelea kuziamini Marekani na Ulaya

Ayatullah Araki, akiendelea kuzungumzia mabadiliko ya kikanda na kimataifa, alisema: Kipindi cha kupewa muhula, kwa mujibu wa kanuni za Mwenyezi Mungu na pia kwa kuzingatia hali iliyopo katika eneo hili, hakitadumu kwa muda mrefu. Kwa hiyo, watawala wanapaswa kurekebisha mwenendo na sera zao kabla ya fursa hiyo kumalizika.

Akizungumzia kupungua uwezo na nafasi ya Marekani katika mizania ya dunia, aliongeza: Enzi ya watawala wa kusini mwa Ghuba ya Uajemi kutegemea nguvu za Marekani na Ulaya imekwisha. Leo, Marekani yenyewe inatafuta wa kuiunga mkono na msaada inayouhitaji, inaomba msaada kutoka kwa nchi za Ulaya, inanyoosha mkono wa kuomba msaada kwa Urusi na hata inaziomba nchi ndogo pia ziiunge mkono.

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi, akisisitiza kwamba hali ya nguvu ya Marekani imebadilika ikilinganishwa na ilivyokuwa hapo awali, alieleza: Nguvu ya Marekani katika nyanja mbalimbali inakabiliwa na changamoto kubwa, na haiwezi tena kuchukuliwa kuwa ni nguvu ambayo nchi za eneo hili zinaweza kutegemea uungaji mkono wake wa uhakika.

Jamhuri ya Kiislamu imeipiga Marekani pigo kubwa katika vita vilivyolazimishwa dhidi yake

Akizungumzia vita vilivyolazimishwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alisema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika vita vilivyolazimishwa dhidi yake, iliipiga Marekani pigo kubwa, kiasi kwamba nchi hiyo haitaweza kurejesha kwa urahisi hali na nafasi yake ya awali. Wamarekani wanajitahidi kuficha athari na matokeo ya mapigo hayo katika uwanja wa propaganda, na hawataki kuruhusu ukweli ujulikane ipasavyo mbele ya maoni ya umma, lakini ukweli huo utaanza kudhihirika hatua kwa hatua.

Akieleza kwamba athari za mabadiliko haya zinaweza kuonekana kwa watazamaji na wachambuzi, alibainisha: Mtu yeyote ambaye haoni athari na matokeo ya mapigo haya, inapaswa kutiliwa shaka kuhusu kiwango cha uelewa na utambuzi wake wa hali halisi iliyopo.

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi, akizielekeza kauli zake kwa nchi za Kiarabu za eneo hili, alisisitiza: Mnapaswa kufahamu kwamba Marekani ya leo si ile nguvu mnayoweza kuiamini na kujenga mustakabali wenu kwa kutegemea uungaji mkono wake, nguvu pekee ya kweli iliyobaki kwenu ni nguvu ya wananchi wenu wenyewe.

Ayatullah Araki, akiendelea kutoa pendekezo kwa watawala wa nchi za kusini mwa Ghuba ya Uajemi kuhusu kubadili mwelekeo wa sera zao za kikanda, alisema: Ikiwa mnataka kuwa na nguvu na ushawishi katika eneo hili, kuna njia rahisi zaidi na yenye ufanisi mkubwa zaidi, nayo ni kuwahudumia wananchi wa eneo hili na kusaidia maendeleo na ustawi wa nchi za Kiislamu.

Mwalimu wa masomo ya juu ya Hawza ya Qum aliongeza: Badala ya kutuma silaha kwa maadui wa wananchi wa Lebanon na kuweka mazingira ya kufanyika uhalifu dhidi ya wananchi wa nchi hiyo, nendeni kuisaidia Lebanon na, kwa kutumia rasilimali na utajiri mlionao, ijengeni upya na kuendeleza maeneo ya kusini mwa Lebanon.

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi, akikosoa sera za uhasama dhidi ya wananchi wa Yemen, alisema: Kwa nini mnapigana na Yemen? Kwa nini mnatumia mitaji na uwezo wenu katika vita dhidi ya wananchi wa nchi hii? Badala ya kutumia rasilimali za kifedha katika njia ya vita na uharibifu, jengeni miundombinu ya kiuchumi, kielimu na kiutamaduni ya Yemen.

Alisisitiza: Ikiwa mtawasaidia wananchi wa eneo hili na kuchukua hatua katika njia ya maendeleo na ustawi wao, badala ya uadui na makabiliano, mtatengeneza mazingira ya urafiki na ushirikiano. Mataifa ambayo leo huenda yakawa na misimamo dhidi ya baadhi ya sera zenu, yakishuhudia tabia zenu za nia njema na huduma za dhati, yanaweza kubadilika na kuwa marafiki na kuwaunga mkono.

Njia pekee ya tawala kudumu ni kupata imani na kuungwa mkono na wananchi

Ayatullah Araki, akizungumzia wasiwasi wa baadhi ya watawala wa eneo hili kuhusu kuhifadhi madaraka na kuendeleza tawala zao, alisema: Watawala wa kusini mwa Ghuba ya Uajemi, ikiwa wanataka kubaki madarakani, wanapaswa kuwasaidia wananchi wao na badala ya kutegemea nguvu za kigeni, wapate imani ya wananchi wao.

Aliendelea kusema: Ikiwa wananchi watakuwa pamoja nanyi na kuiunga mkono serikali yenu, hata wale wanazuoni ambao leo hukumu za kuuawa kwao zinatolewa, watakuwa watu wa kwanza kuwaunga mkono; kwa sababu wanazuoni wa dini wanatafuta kheri na maslahi ya wananchi, na ikiwa serikali zitaelekeza mwenendo wake katika kuwahudumia wananchi, hakutakuwa na sababu ya kukabiliana nazo.

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi, akieleza kwamba uungaji mkono wa wananchi kwa serikali unategemea tabia na utendaji wake, alisema: Ikiwa mtatenda mambo yenye manufaa kwa wananchi, kuweka uwezo na rasilimali zenu kwa ajili yao, na kuwaruhusu wanazuoni wa Umma kuzungumza nanyi na kueleza mitazamo yao, mazingira ya kupata imani na ushirikiano wa wananchi yatajitokeza.

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza aliongeza: Vilevile, mnapaswa kuwapa wananchi fursa ya kushiriki katika kufanya maamuzi na masuala ya kiutawala ya nchi. Wananchi wanapaswa kuwa na uwezo wa kutoa maoni, kupiga kura, kukosoa na kushiriki katika kuamua hatima ya jamii yao. Katika mazingira kama hayo, wananchi wataiunga mkono serikali na watakuwa tegemeo lake kuu.

Ayatullah Araki alibainisha: Serikali hazipaswi kuogopa ushiriki wa wananchi wala utoaji wa mitazamo ya wanazuoni na wanafikra; kwa sababu ikiwa sera zitakuwa katika mwelekeo wa kulinda maslahi ya umma na kuhakikisha haki za wananchi, uungaji mkono wa wananchi utajitokeza wenyewe.

Jamhuri ya Kiislamu kuwaunga mkono wananchi wanaoinuka dhidi ya dhuluma na udikteta

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, akifafanua msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na mabadiliko ya ndani ya nchi za eneo hili, alisema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiingilii masuala ya ndani ya nchi yoyote; lakini ikiwa wananchi wataamka na kuinuka kwa ajili ya kujikomboa kutoka katika dhuluma na uonevu wa watawala wao, bila shaka Jamhuri ya Kiislamu itawaunga mkono.

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi aliongeza: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikiwaunga mkono wananchi wenye msimamo thabiti na mataifa yanayoamka na kusimama dhidi ya dhuluma, uonevu na watawala madhalimu. Katika njia hii, wananchi wa nchi za eneo hili pia watanufaika na uungaji mkono huo.

Alisema: Tunatumaini kwamba ujumbe huu utawafikia wananchi na watawala wa Kuwait na nchi nyingine za eneo hili, na kwamba watazingatia umuhimu wa kurekebisha mwenendo wao, kuheshimu haki za wananchi na kukomesha sera za ukandamizaji.

Kosa la Sheikh Hussein al-Matouq ni lipi isipokuwa kuwahudumia, kuwafundisha na kuwaongoza wananchi?

Ayatullah Araki, akiendelea kuzungumzia shakhsia ya kielimu na kijamii ya Sheikh Hussein al-Matouq na kutolewa hukumu ya kifo dhidi ya mwanazuoni huyo wa dini, alisema: Leo tunapaswa kuwauliza watawala wa Kuwait: Kosa la mwanazuoni huyu mpambanaji, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Hussein al-Matouq, ni lipi?

Akisisitiza umuhimu wa kuchunguza kwa haki na uadilifu historia ya kielimu, kiutamaduni na kijamii ya shakhsia hii ya kidini, aliongeza: Muulizeni mwanadamu yeyote mwenye uadilifu kuhusu utendaji na historia ya mwanazuoni huyu.

Je, katika historia yake kuna jambo lolote isipokuwa kuwahudumia wananchi, kutoa elimu na malezi, pamoja na kuiongoza jamii? Inatarajiwa kwamba watawala wa Kuwait watapitia upya ya uamuzi huu, warejee katika busara na hekima, na kufuta hukumu ya kifo dhidi ya mwanazuoni huyu mpambanaji haraka iwezekanavyo.

Kufutwa hukumu ya kifo dhidi ya Sheikh Hussein al-Matouq ni matakwa ya wananchi wa Kuwait na ulimwengu wa Kiislamu

Akisisitiza kwamba; kufutwa hukumu ya kifo dhidi ya Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Hussein al-Matouq ni takwa muhimu, alibainisha: Kufutwa hukumu hii ni matakwa ya wananchi wote wa Kuwait na ulimwengu wa Kiislamu, na tunatumaini kwamba watawala wa nchi hiyo watachukua hatua katika suala hili haraka iwezekanavyo.

Ayatullah Araki, mwishoni alisema: Takwa letu haliishii katika kesi ya Sheikh Hussein al-Matouq pekee, bali pia tunadai kuachiliwa huru na kuondolewa vikwazo dhidi ya wafungwa wote katika nchi za Kuwait, Bahrain na Saudi Arabia. Tunatumaini kwamba watawala wa nchi hizi watazipitia tena sera zao na kuweka mazingira ya watu hawa kuachiliwa huru na kurejea katika jamii.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha